1 Chronicles 16

Sanduku Lawekwa Ndani Ya Hema

1 aWakaleta Sanduku la Mungu na kuliweka ndani ya hema ambalo Daudi alikuwa amelisimamisha kwa ajili yake, na wakatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani mbele za Mungu. 2 bBaada ya Daudi kumaliza kutoa hizo sadaka za kuteketezwa na hizo sadaka za amani, akawabariki watu katika jina la Bwana. 3Kisha akamgawia kila Mwisraeli mwanaume na mwanamke mkate, andazi la tende na andazi la zabibu kavu.

4 cAkawaweka pia baadhi ya Walawi ili wahudumu mbele ya Sanduku la Bwana kufanya maombi, kumshukuru na kumsifu Bwana, Mungu wa Israeli: 5Asafu ndiye alikuwa mkuu wao, akisaidiwa na Zekaria, Yeieli, Shemiramothi, Yehieli, Matithia, Eliabu, Benaya, Obed-Edomu na Yeieli. Hawa ndio wangepiga zeze na vinubi, Asafu angepiga matoazi, 6nao Benaya na Yahazieli makuhani, ndio wangepiga tarumbeta mara kwa mara mbele ya Sanduku la Agano la Mungu.

Zaburi Ya Daudi Ya Shukrani

(Zaburi 105:1-15; 96:1-13; 106:1, 47-48)

7 dSiku ile, kitu cha kwanza Daudi alichofanya ni kumkabidhi Asafu na wenzake zaburi hii ya shukrani kwa Bwana:
8 eMshukuruni Bwana, liitieni jina lake;
wajulisheni mataifa yale aliyoyatenda.

9 fMwimbieni yeye, mwimbieni yeye sifa;
waambieni matendo yake yote ya ajabu.

10 gLishangilieni jina lake takatifu;
mioyo ya wale wamtafutao Bwana na ifurahi.

11 hMtafuteni Bwana na nguvu zake;
utafuteni uso wake siku zote.

12 iKumbuka matendo ya ajabu aliyoyafanya,
miujiza yake na hukumu alizozitamka,

13 enyi wazao wa Israeli mtumishi wake,
enyi wana wa Yakobo, wateule wake.


14 jYeye ndiye Bwana Mwenyezi Mungu wetu;
hukumu zake zimo duniani pote.

15 Hulikumbuka agano lake milele,
neno ambalo aliamuru, kwa vizazi elfu,

16 kagano alilolifanya na Ibrahimu,
kiapo alichomwapia Isaka.

17 lAlilithibitisha kwa Yakobo kuwa amri,
kwa Israeli liwe agano la milele:

18 m“Nitakupa wewe nchi ya Kanaani
kuwa sehemu utakayoirithi.”


19 nWalipokuwa wachache kwa idadi,
wachache sana na wageni ndani yake,

20 walitangatanga kutoka taifa moja hadi jingine,
kutoka ufalme mmoja hadi mwingine.

21 oHakuruhusu mtu yeyote awaonee;
kwa ajili yao aliwakemea wafalme, akisema:

22 p“Msiwaguse niliowatia mafuta;
msiwadhuru manabii wangu.”


23 qMwimbieni Bwana dunia yote;
tangazeni wokovu wake siku baada ya siku.

24 rTangazeni utukufu wake katikati ya mataifa,
matendo yake ya ajabu miongoni mwa mataifa yote.

25 sKwa kuwa Bwana ni mkuu,
mwenye kustahili kusifiwa kuliko wote;
yeye ni wa kuogopwa kuliko miungu yote.

26 tKwa maana miungu yote ya mataifa ni sanamu,
lakini Bwana aliziumba mbingu.

27 Fahari na enzi viko mbele yake;
nguvu na utukufu vimo patakatifu pake.

28 uMpeni Bwana, enyi jamaa za mataifa,
mpeni Bwana utukufu na nguvu,

29 mpeni Bwana utukufu
unaostahili jina lake.
Leteni sadaka na mje katika nyua zake;
mwabuduni Bwana katika uzuri wa utakatifu wake.

30 vDunia yote na itetemeke mbele zake!
Ulimwengu ameuweka imara; hauwezi kusogezwa.

31 wMbingu na zishangilie, nchi na ifurahi;
semeni katikati ya mataifa, “Bwana anatawala!”

32 xBahari na ivume, na vyote vilivyomo ndani yake;
mashamba na yashangilie, na vyote vilivyomo ndani yake.

33 yKisha miti ya msituni itaimba,
itaimba kwa furaha mbele za Bwana,
kwa maana anakuja kuihukumu dunia.


34 zMshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema;
upendo wake wadumu milele.

35 aaMlilieni, “Ee Mungu Mwokozi wetu, tuokoe.
Tukusanye tena na utukomboe kutoka kwa mataifa,
ili tuweze kulishukuru jina lako takatifu,
na kushangilia katika sifa zako.”

36 abAtukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli,
tangu milele na hata milele.

Nao watu wote wakasema, “Amen,” na “Msifuni Bwana.”

37Daudi akamwacha Asafu na wenzake mbele ya Sanduku la Agano la Bwana ili wahudumu humo mara kwa mara, kulingana na mahitaji ya kila siku. 38 acPia akamwacha Obed-Edomu pamoja na wenzake sitini na wanane wahudumu pamoja nao. Obed-Edomu mwana wa Yeduthuni na pia Hosa walikuwa mabawabu wa lango.

39 adDaudi akamwacha kuhani Sadoki pamoja na makuhani wenzake mbele ya hema ya ibada ya Bwana katika mahali pa juu pa kuabudia huko Gibeoni 40 aeili kutoa sadaka za kuteketezwa kwa Bwana kwenye madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa mara kwa mara, asubuhi na jioni, sawasawa na kila kitu kilichoandikwa katika sheria ya Bwana ambayo alikuwa amempa Israeli. 41 afWaliohudumu pamoja nao walikuwa Hemani, Yeduthuni na wale wote waliochaguliwa na kutajwa kwa jina kumpa Bwana shukrani, “Kwa maana fadhili zake zadumu milele.” 42 agHemani na Yeduthuni walikuwa na wajibu wa kupiga tarumbeta, matoazi na kutumia vyombo vingine kwa ajili ya nyimbo za sifa kwa Mungu. Wana wa Yeduthuni waliwekwa langoni.

43 ahKisha watu wote wakaondoka, kila mmoja akarudi nyumbani kwake, naye Daudi akarudi nyumbani kuibariki jamaa yake.
Copyright information for SwhKC